17/05/2017

Sayansi "ngumu" kuhusu Afrika inavyofanyika... Uzunguni !


Ni miaka mingi sasa nimekuwa natafuta vitabu vya sayansi vinavyozungumzia bayoanuai na ikolojia ya bara ya Afrika. Nimetembelea vyuo vikuu vyote vya Afrika Mashariki, maktaba yote pamoja na maduka mengi ya vitabu, wala sijapata kuona vitabu vilivyoandikwa na wana sayansi wa kiafrika, katika kiswahili ama kiengereza (licha ya kifaransa). Sielewi kwa nini hapa Afrika inaelekea kwamba maprofesa na wana sayansi takriban wote hawapendi mazingira na nchi yao. Kwangu ni kitandawili kikubwa. Haileweki. 


Basi hapo chini nimebandika picha ya kitabu ninachosoma siku hizi kuhusu bayolojia na ikolojia ya mamalia ambao wanaishi Afrika. Vitabu hivyo — kwa sababu ni majuzuu sita (zaidi ya kurasa 3500) — ni vya ajabu kweli. Hivyo nimeweka pia video kuhusu mwandishi andamizi ambaye amejitolea katika kutunga toleo hilo kubwa.


                             


08/04/2017

Kiswahili cha kisasa kipo ?


Mtu akivinjari katika tovuti na blogu mbalimbali za kiswahili huambiwa kila muda kwamba kiswahili kinazidi kukua. Kwamba kimepevuka, kimepanuka kiasi cha kustahili sasa kujivuta katika medani ya lugha nyingine tajiri za duniani. Maoni haya hayana msingi kwangu. Ni ajabu kubwa, labda kwa sababu natumia lugha nne katika kusoma vitabu, jambo ambalo linachangia sana kuchonga akili ya mtu apate kuchanganua utajiri na umaskini wa lugha. Lakini si hivyo tu. Kila wiki, vitabu kadhaa huwa vinanihangaisha, si riwaya peke yake, bali hasa ni vitabu vya sayansi, vile vyenye uketo wa ndani katika taaluma mbalimbali, ikiwemo etolojia, bayolojia ya wanyama na vidudu fulani, ikolojia na kadhalika. Sina budi kusema kwamba nimebahatika kuzaliwa katika nchi yenye lugha tajiri (kwa maana ni lugha yenye historia ndefu) kitu ambacho kinanipambazukia niwe makini na wenye ari katika matumizi tofauti ya lugha yetu, ikiwemo ushairi na sayansi. Na leo hii, nikitaka kusoma kitabu cha sayansi, bila shaka nitakigeukia kifaransa au kiengereza, lakini nitakitupilia mbali kiswahili. Kitabu changu nachosoma siku hizi kinaitwa « Kutokuwa na kumbukumbu katika kupambana na ubadilifu wa mfumo wa ikolijia… » Na ni kitabu kiuzwacho katika duka lolote Ulaya. Huna haja ya kuwa msomi au Profesa mkwasi wa Chuo Kikuu, kwa sababu mtu yeyote mwenye elimu atakuwa hana tatizo lolote kukisoma. Hata kama dhana na msamiati mgumu zimo, lakini kwa kuwa shule za Ulaya ni shule zenye maana, mtu yeyote atawahi kupambana nacho. Lakini je, Uswahilini mtindo huo umeshapambazuka ? Kwani mtu anaweza kuandika insha au makala kuhusu, kwa mfano, tabia ya kuzaliana kwa mbwa msitu na athari za uchafuzi wa mazingira juu ya tabia hiyo ? Mfano mwingine, siku hizi tunazumgumzia sana mambo ya mabadiliko ya tabia nchi. Lakini viko wapi vitabu vya ndani kuhusu hoja hiyo, kwa kiswahili ? Wangapi, katika wananchi wale waliotimiza kidato cha sita, wataibuka hapo kuwakilisha mjadala uliopo siku hizi katika vikosi vya wana sayansi duniani, huku wakitumia kiswahili ?

Nakumbuka, miaka mingi nyuma, katika miaka themanini ya karne iliyopita, nilipofikwa na jamaa aliyenigaia diwani ya Abdilatif Abdalla iitwayo Sauti ya dhiki. Niliposoma kitabu hicho, wakati ule, raha ilinikunjukia jinsi kiswahili chake kilivyonakshiwa kwa umahiri. Kitabu hicho kilichapishwa mwaka 1973 na kilitangulizwa na dibaji ya bwana mmoja ambaye hakunyimwa nafasi nzuri ya kuchomekea lake. Naomba nitoe baadhi ya maneno yake ili mtu apate kuelewa vizuri nachokusudia kusema hapo, hasa kuhusiana na utaratibu ule uliozidi, kuanzia miaka hiyo ya 70, kukwamisha lugha ya kiswahili isije ikawa lugha ya kisasa. Huyo mheshimiwa, kwa jina lake Shihabuddin Chiraghdin, aliandika :

« (lugha ya kiswahili) tuikuze kwa kuzichanganya janibu zote za kiswahili ; tusiivize kwa kushikilia zile zile ndweo na ndezi za kikoloni, tukawa na lazima na urathi wao. Njia moja ya kuikuza, kuitukuza na kuivyaza lugha ya kiswahili ni kupatikana maandishi kama haya ya Abdilatif — yatoke janibu zote. »

Niliposoma dibaji hiyo kwa mara ya kwanza, nilifurahi sana. Siwezi kuficha kwamba kitabu hicho kilinihimiza sana niendeleze juhudi zangu za kusoma zaidi kiswahili. Lakini leo, nimerudi mkuse, kama tunavyosema katika kisongo kilichoparauka katika « janibu » ya Kilwa. Kwani miaka zaidi ya 45 imepita sasa kutoka 1973. Na maua yale yaliyotarajiwa kuvyaa, kama alivyonena bwana huyo, yako wapi ? Vitabu vile vya mashairi viko wapi ? Vitabu vingapi vinachapishwa kila mwaka ili wasomaji wa kiswahili wapate « kucheza kwa mdundo wa kiafrika » ? Mboni ukapa ukaenea sana ikawa miti yote imelanika (kikilwa hicho !) ? Aidha, kukuza lugha katika taaluma yake mojawapo ni vizuri sana, lakini je, taaluma zile nyingine ? 

                                                               

Tuondokane na bwana huyo mkubwa tumgeukie mwingine. Hapa naomba kutaja kitabu cha marehemu rafiki yangu Alain Ricard, katika kitabu chake kizuri kihusucho mwandishi Ebrahim Hussein ambaye anachukuliwa (na sisi wawili) ni mwandishi mzuri sana katika waandishi wote katika lugha ya kiswahili. Mwandishi huyo aliwahi kuandika tamthilia nyingi ikiwemo Kijinkitile na Mashetani. Basi vijana wa siku hizi waelewe vizuri, kwa sababu si wengi kati yao waliobahatika kwenda shuleni, kwamba msanii huyo maarufu alipondwa na kuzomewa na vichwa vile kwa sababu eti msanii huyo anatumia kiswahili kigumu. Mimi Mzungu niliyesoma vitabu vile Mashetani na Kijinkitile, sijapata taabu kuvielewa. Mboni mzawa mwenye uzalendo mwingi havielewi ? Wacha dhana ya utamaduni, ambayo si hoja noma katika kusoma na kuelewa kitabu chochote cha fasihi, nini maana yake, nini sababu yake ya kusema kwamba « kitabu cha fasihi » si kizuri kwa kuwa si rahisi kukielewa ? Kwa nini Ebrahim Hussein alitupwa na wasomaji wake baada ya kutolewa kwa Mashetani ? Jibu tunalipata katika kitabu cha Alain Ricard aliyebobea katika kuchanganua kazi za uhakiki (au ni hukumu ?) zilizoletwa na baadhi ya « wasomi » wa enzi ile, katika miaka ya sabini. Mfano bwana Kiango ndiye aliyeleta baadhi ya mishale iliyofumwa na kutoswa katika sumu ya siasa dhidi ya michezo ya Ebrahim Hussein wakati ule. Ni vizuri kuitaja hapo angalau tupate kukumbuka utaratibu ule ulioleta kusambaratika kwa fasihi kuanzia miaka themanini :

« Kwa sababu ya umuhimu wa mchezo huu kwa kila Mtanzania, ndiyo hapa namlaumu mwandishi kwa kuandika Mashetani kama alivyouandika. Kwa sababu ni watu wachache watakaouelewa kwa urahisi. Kwa wengi, unakuwa ni kama kujaribu kuvunja chuma kwa meno »

Vijembe kama hivi viko vingi katika maandishi ya « kitaalamu » ya miaka ile Tanzania. Hakuna mtu hapo kunyosha mkono na kuuliza : « huyo bwana Kiango ameandika nini mwenyewe, amefanya nini ili kujishaua kiasi hicho ? ». Lakini si ishu. Kikubwa hapo ni kwamba tunaambiwa tusadiki maneno ya bwana mkubwa huyo ambaye alishindwa, kama Maprofesa wengi wa chuo kikuu cha wakati ule, kuzikabili kazi za fasihi kama ipasavyo, yaani kama sekta ya ubunifu unaotakiwa kupimwa kwa kutumia mbinu na mikabala ya kiujumi peke yake. Bwana Kiango angeibuka katika mjadala ule wa ubora wa vitabu vya Ebrahim Hussein huku akijadilia sifa za kiujumi za michezo yake, tungemtukuza sana. Lakini kipindi kile cha usanii wa Ebrahim Hussein kilikuwa enzi ya Ujamaa ambao tayari tumeshang’amua kwamba ulikuwa ni aina ya ukoministi, ingawa ukoministi wa kiafrika.


Hatuwezi kulaumu wananchi wa Afrika Mashariki, na mimi nitahisi kama sitawatendea haki wenzangu niliokaa nao miaka mingi, vijijini na porini (kilingeni na utagalani), kwa kuwa ndio wao wanaojua kiswahili cha ndani Tanzania na Kenya. Si vichwa vile vya mijini ambao maandishi yao yanafanana na visuguzi na vikwabuzi vya kufutilia mbali kiswahili kile cha ndani, kile ambacho kisuguliwacho na dodoki na "mafuta ya nyonyo" ya kienyeji. Najitahidi, kila nikiandika kwa kiswahili-hicho-cha-mipasho (kipendezwacho na madikteta), kujizuia nisije nikachanganya kile nachozoea nacho, ambacho kimesheheni msamiati na istihali za kienyeji, si lahaja si lafudhi, ili wasomaji wangu wapate kunielewa. Lakini kujisahilisha ni wajibu kwa mwenye blogu, si kanuni wala sheria ya mwana fasihi. Kiswahili kinachochukuliwa ni kisanifu ndicho kile watumiacho wale vichwa na wanene wa mjini ambao hawajui kinachoendelea vijijini kwao. Ndio wao wanaojitahidi kudhibiti kisichofaa ili jamii ifuate "maadili" na "nyaadhi" za kisiasa.  Fasihi itawezekana katika muktadha huu wa mwafaka ? Bila shaka, kwa misaada ya "vihiyo" vile vya Chuo Kikuu na "vitaalamu" vya gengeni. Si wana nguvu na nyenzo za kuonea mburumatari na waandishi waasi wanaoleta vurugu ya kibinafsi katika jamii ? La kuchekesha ni kuona kwamba hawa vichwa — licha ya kuwazomea waandishi — mara nyingi huona kwamba kiswahili hicho kisanifu kililetwa na wakoloni. Si wazee walisema « kikulacho ki nguoni mwako » ?


Kuhusu Alain Ricard : HAPA 

Kuhusu Ebrahim Hussein : HAPA (katika lugha ya "vihiyo"), HUKU10/03/2017

Serengeti na mbuga nyingine : urithi utakaopotea ?


Serengeti ni bidhaa. Lakini pia ni jamvi la wageni. Kwetu mtu haoni sababu ya kuhifadhi mbuga iliyojaa wanyama waharibifu. Hivyo mihadhara na hafla nyingi za kienyeji ziitishwe kuamsha akili za watu ili wote waelewe kwamba wanyama wale ni fedha. Kama hawana faida, wana tija gani zaidi ya hiyo ? Bayoanuai ? Acha dhana hiyo ya kizungu. Ni fedha tu. Hivyo tumpembejee mzungu na mfadhili mwema atuletee mshiko tu. Nasi tuwe na uwezo ule wa kuchapisha ramani na bango. Bure ghali. Watalii wasipotee ndani ya pori hiyo kubwa. Si mzungu ndiye aliyeturithisha hifadhi hizo ? Yeye ndiye anayeranda ndani ya mbuga. Sisi Waafrika, hatuna mpango huo. Ndio wao wanaotikita game drive. Sisi jamii yetu kutungamana tu, kushirikiana na kupeana. Burudani yetu ni human drive.


Mzungu hajui kwamba falsafa yetu imekolea viungo vyenye ladha ya maovu. Mfano Serengeti. Yeye mzungu anatuhamasisha tuwe makini kabisa na hifadhi hiyo iliyowekwa katika orodha ya Unesico. Itunzwe vizuri. Sawa, lakini ina gharama. Na sisi ndio tutakaochuuza sehemu hiyo ya Tanzania katika mnada. Tufaidike na sisi. Wazungu wana utamaduni na itikadi ya mazingira. Eti wale hawapendi sisi tujenge barabara kuu ndani ya hifadhi. Watu wasinune. Hilo sakata kubwa ni faida yetu basi. Fidia itozwe hapo. Uendeshaji sisi, mtaji wao ! Yaani miundombinu, barabara na maslahi yote wawekeze wao ! Kama wanapenda mbuga iwepo. Tusisahau wazee waliposema, baniani mbaya, kiatu chake dawa. Wakipenda wasipende, tutajenga viwanda, boma, gridi za umeme, kinu cha kinuklia, treni na mambo mengine ! Ndani ya mbuga. Watakoma ! Si tumeshaanza na Selous ? Raha ya maovu !

27/01/2017

Kuzaa wengi : utamaduni wa urijali au kasumba ?


Kabla ya enzi ya ukoloni, si miaka mingi nyuma, Afrika ilikuwa ni eneo la dunia ambalo lilikuwa halina watu wengi. Kwa sababu hiyo, tunaweza kuchukulia kuwa maliasili ya bara hiyo, kwa wakati ule, ilikuwa haimaliziki. Na katika jamii zote za Afrika, kama ilivyokuwa bara nyingine kabla ya kuzidiwa na wakaazi wengi, watu waliishi kwa kuchuma maliasili kwa kadiri wawezavyo. Kuanzia karne 19, hususan wakati wa majilio ya wakoloni, bara hiyo ilijaaliwa — ama ililaaniwa — kukumbwa na ongezeko la watu, haswa kwa msaada wa utibabu ulioletwa na wakoloni. Idadi ya watu hapo ndipo ilipata kuongezeka kwa kiasi kikubwa.

Siku hizi, idadi ya watu bara ya Afrika inaendelea kuongezeka kwa kiwango kikubwa kushinda bara zote za dunia ambapo mwendo wa ongezeko la watu umeshaanza kulegea hadi kushuka kama ilivyo katika baadhi ya nchi zilizotajirika katika mawanda ya elimu (mfano Japan). Kadiri kiwango cha elimu kinavyoshuka katika nchi yoyote, ndipo ongezeko la watu unaposhika kasi. Tunayo mifano mingi ya nchi za Afrika magharibi kama vile Nigeri au Chadi ambapo kasi ya kuongezeka kwa watu imepungua kidogo ikakua tena hivi karibuni baada ya kusambaratika kwa asasi za elimu (shule na vyuo vikuu). Kwa kifupi, ongezeko la watu linaakisi kiwango fulani cha ukosefu wa elimu. Kote duniani, katika historia ya nchi zote, ujinga ulikuwa — na unazidi kuwa, kwa nchi nyingi —, ni mchango na msukumo mkubwa sana katika kuongezeka kwa watu, kwanza katika familia, pili katika jamii kwa jumla.


Uwiano huo kati ya kiwango cha elimu na kasi ya ongezeko la watu unamaanisha kwamba maendeleo katika sekta ya uchumi si kigezo cha kutilia maanani katika kupunguza kasi hiyo. Uchumi si kitu. Mifano tunayo mingi tu. Katika nchi kadhaa za kiarabu, watu huzaa watoto wengi hata kama ni mabilionea. Nao ni matajiri kiuchumi lakini pia ni watu ambao wengi hawana elimu. Nchi nyingi za dunia ya leo, kama vile India na China, ambazo zinachukuliwa ni mataifa makubwa kiuchumi, bado hazijaingia katika kikosi cha nchi zenye ustaarabu katika kuthabiti na kusimamia kuongezeka kwa wakaazi wao, kwa sababu mfumo wa elimu umekuwa dhaifu. Licha ya hayo, nchi hizo bado hazijakomesha umaskini wao ambao kwa kweli umekithiri miaka hii ya hivi karibuni.

Na dalili za kuwa na elimu zinapatikana katika takwimu kadhaa hususan katika tathmini zinazofanyika katika sekta ya ubunifu kama vile vyeti vichapishwavyo kila mwaka katika kila nchi. Na sitakosea nikisema kwamba hakuna ukanda mwingine duniani ambao umeponza na kuzorotesha maendeleo ya sekta hiyo kama ilivyo ukanda wa Afrika. Ni ya kuhuzunisha kwa kuwa bara ya Afrika kwa jumla inaendelea kudidimia kielimu — ingawa teknolojia na miundombinu imepandikizwa ikamea barabara —, baada ya kupata uhuru takriban miaka 60 nyuma, na kujizongoresha akilini rubega ya visingizio vya kisiasa wakati dunia nzima inahitaji kuamsha akili za watu wote tukashirikiane katika kupambana na maafa na janga zijazo.

Hapo naomba (ashakum) kusogeza takwimu chache tu — najua ukweli unauma — ili kusisitiza kilicho wazi kabisa katika sekta ya elimu na ubunifu (wala ubunifu hauambatani na uchumi) : mwaka 2009, dunia nzima imerekodi ikahalilisha vyeti takriban 166 000 katika ubunifu na uvumbuzi ; katika vyeti hivyo vyote, 486 vilipatikana Afrika, ikawa sawa na asilimia 0,3 ya vyeti vyote. Katika 0,3 % hivyo, 90 % vilipatikana Afrika kusini, lakini katika matokeo haya, 80% vilibebwa na Waafrika weupe na 10% na Waafrika wahindi (takwimu hizo zinazoakisi aina ya ukabila na uhasama zingekuwa hazina maana katika nchi yoyote ya dunia, ambapo raia hana rangi, lakini inajulikana wazi kwamba Afrika kusini ni nchi ambayo haijaondokana na ubaguzi wa rangi ingawa jina la apartheid limefutwa). Mwaka huo huo wa 2009, Moroko ndiyo nchi iliyopata 10% ya vyeti vilivyobaki pamoja na Misri iliyopata 41%. Ya kusikitisha sana, hasa msomaji ukilinganisha takwimu hizo na zile za nchi yoyote ya Amerika kusini na Asia.

Maelezo hayo hayana ubabe wala kejeli. Yana ukweli tu. Mtu akivinjari katika tovuti mbalimbali ya kibongo pia atagundua ukweli huo. Kwa mfano nakumbuka wakati waziri mkuu Mizengo Pinda alipotoa onyo kali kuhusiana na ongezeko la watu Tanzania. Ikawa matope, matusi, mawe, kibesi na viwembe. Nusura mheshimiwa kupigwa kitutu. Baadhi ya vijembe vile nimevi-kopy (?) hapo kama ifuatayo (hapo sijakosoa makosa ya kiswahili, au ni mategu ?) :

« Tusipende kukopy kila kitu mzungu anachotuletea mzungu kaleta family planning sasa ndio imekua nyimbo kila siku »

« Tatizo viongozi wetu hawasomi na wanakalili mitizamo hasi ya watu wa magharibi »

« Uzazi wa mpango uzazi wa mpango, uhuni wa wazungu huu viongozi wetu wanauimba kama kasuku, no thinking »

Wadau hawa ni wakweli kabisa. Wazungu ndio wanaohusika katika kuleta « mawazo hasi, madudu mabaya na maadili ya kijinga kuhusu jinsia, kuzaa nje ya ndoa na uzazi wa mpango ». Ishu hiyo haina noma (objection) kwa kuwa inajulikana tangu zamani ya kale kwamba dhana hasi ni kichocheo kikubwa cha ujuzi, falsafa, sayansi na elimu. Si Wazungu wamepiku katika sayansi na udaktari tangu enzi na enzi ? Si uovu umo katika uzuri (kama msomaji umezubaa, soma Ayubu katika Biblia) ? Ningekuwa na nafasi hapo kutaja waandishi na wasayansi maarufu (katika wale ambao walichangia pa kubwa sana katika kuinua maisha ya binadamu) waliodhihaki wenye maoni chanya, nadhani maandishi yangu yangejaza maktaba nzima. Kikubwa hapa ni jinsi dhana chanya ilivyo ni msingi wa muono na mtizamo wenye ubwege. Lakini si hoja yangu ya leo.

Hapo najiuliza : uzazi huo wa ulemete (kutunga mimba na kuwa mtoto mwingine mkononi) na kuzaa kama ncha ya kimondo kweli ungekuwepo leo hii kama wakoloni wasingefika Afrika ? Wao ndio walioleta chanjo, dawa, hospitali na sayansi ya kuongezea miaka ya kuishi na kupata watoto wengi (nisitaje uovu wao wa aina nyingine). Tunajua wazi kwamba wasingekuja, watu wangeendelea kupambana na maafa makubwa kama vile maambukizi na kifo cha mapema. Tangu walipotokezea na sayansi na udaktari zao (mbaya ?) umri wa wastani wa kuishi umeongezeka, vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano vimepungua sana, na hali kadhalika. Yote hayo ni katika maendeleo ya vifaa na mbinu ziletwazo kutoka nje. Lakini je, tabia, mienendo na hali ya kupambana na uzazi, kweli zimebadilika ? Isitoshe, wengi husema kwamba kuzaa ni katika utamaduni wa kiafrika. Hapo pia kauli hiyo haina kichwa wala miguu kwa kuwa dunia nzima, penye ujinga, pana watoto wengi ! Si Afrika, si Ulaya, kote duniani. Msukumo mkubwa wa kuzaa huwa ni urijali na kutokuwa na upeo wa akili, hususan ni ubabe na ubaradhuli wa kiume, mwanamke mja mzito asije akawania elimu na uwezo wa kupigania haki zake.